Maneno afichua siri Kliniki ya bure

Maneno afichua siri Kliniki ya bure

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno amefichua siri ya uwepo wa Kliniki ya Kisheria bure kuwa ina lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ili waweze kupata ushauri na msaada wa kisheria kwa urahisi.
Maneno amesema kuwa, zoezi hilo linaendeshwa na ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili wananchi wanaokutana na changamoto za kisheria kila siku ziweze kupatiwa ufumbuzi bure.
Amesema, ofisi hiyo ina jukumu la kuwasimamia mawakili wa Serikali katika ofisi zote za umma ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa manufaa ya umma na Taifa kwa ujumla.
Pia, wanajukumu la kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi ili waweze kupata uelewa wa kutosha na namna bora ya kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
Lengo la kliniki hizi ni kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ili waweze kupata ushauri na msaada wa kisheria kwa urahisi.
Pia,kamati zimeanzishwa ili kutoa ushauri kwa wananchi, watumishi na viongozi wa umma katika kutatua changamoto za kisheria ngazi ya mikoa na wilaya.
Miongoni mwa manufaa ya kamati hizi ni kupunguza migogoro dhidi ya serikali, malalamiko ya kisheria, vitendo vinavyokiuka sheria na taratibu, pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Amesema kwa sasa, kamati hizi zimeshazinduliwa katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Manyara na Simiyu ambapo wananchi zaidi ya 5,000 wamepata usaidizi wa kisheria huku migogoro ya ardhi ikiongoza.
Maneno amesema kuwa kuzinduliwa kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria katika Mkoa wa Dar es Salaam ni mwendelezo wa juhudi na nia ya dhati za Serikali za kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.
“Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam mjitokeze kwa wingi kupata huduma hii ya ushauri wa kisheria inayotolewa bure na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali," amesema Chalamila.
Uzinduzi huo wa kliniki umefanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo uliofanyika Februari 16, 2026  hadi 22 Februari, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Naye, Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Dar es Salaam Albert Chalamila, amewataka Mawakili wa Serikali kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananchi watakaohudhuria Kliniki ya Sheria kwa kutumia lugha nyepesi itakayoeleweka kwa urahisi na wananchi. 
“Katika mkoa huu kuna changamoto nyingi za kisheria kutokana na ukubwa wa mji na mwingiliano wa kibiashara na kijamii, hivyo muwasikilize wananchi na kuwaelimisha kwa lugha nyepesi na rahisi kueleweka,” amesema Chalamila.
Chalamila ameeleza  kuwa uwepo wa kamati hizo utasaidia kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, kutoa huduma za ushauri wa kisheria na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi, kuwawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia utawala wa sheria na kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi.
Vilevile Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo ili waweze kupata huduma za ushauri wa kisheria bure.
RC Chalamila ameipongeza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu zoezi hili muhimu ambalo anasema lina manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema, kutokana na watu wengi kukosa uelewa wa kisheria, katika mazingira ya uraiani pamekuwepo malumbano mengi ambayo huwa yanakosa muafaka, lakini kupitia kliniki hizi na elimu ya kisheria itasaidia wengi kuwa na ufahamu wa kutosha.
Kwa kukosa uelewa wa kisheria, RC Chalamila amesema kuwa,"...ni ukweli kwamba watu wengi katika masuala ya kisheria huwa wanagombana, hivyo nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja na programu hii ambayo itasaidia watu wengi ambao hawana uelewa wa kisheria huko mitaani."
RC Chalamila akizindua huduma hiyo amesema kuwepo kwa huduma bure ya kisheria kutasaidia kupunguza mashauri au migogoro dhidi ya Serikali, malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi, vitendo vya uonevu vinavyovunja sheria na taratibu pia kwa kuwa kuna kamati za mashauri ya kisheria nazo zitatoa elimu ya sheria kwa umma katika kushughulikia changamoto mbalimbali katika maeneo yao.
RC Chalamila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa klinik hiyo ambayo inatimu ya Mawakili wabobevu ambao watakuwa wanatoa huduma za kisheria bila malipo kwa wananchi wote watakaohudhuria katika viwanja hivyo kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dar  es Salaam na Mikoa jirani.
"Migogoro mingi na mikubwa katika Mkoa wa Dar es Salaam huchangiwa na tamaa ya mali ni muhimu kuielimisha jamii kufanya kazi kwa bidii na kujielekeza kumiliki mali na sio urithi wa mali," Alisisitiza RC Chalamila na kuongeza;
“Kwa namna ya kipekee niwashukuru sana wananchi waliojitokeza na kuungana nasi katika uzinduzi wa Kamati hii."

TLS
Mwakilishi wa Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amesema kuwa, moja ya jukumu lao ni kusaidia umma chini ya Kifungu Na.4 cha Sheria ya TLS, hivyo wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi nchini.
Pia, amepongeza uzinduzi wa kamati hiyo huku akiomba zoezi hilo kuwa endelevu ili kuweza kuwahudumia wananchi na makundi mbalimbali nchini.

TPBA
Kwa upande wake,Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA),Wakili Debora Mcharo amesema, chama hicho kinatambua umuhimu wa uzinduzi wa zoezi hili ambalo limeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku wakiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria na ushauri bila malipo.
Amesema, chama hicho kinaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mlezi wa chama chao ili kuhakikisha wanaleta matokeo chanya kwa kuhakikisha wananchi wanapata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria.

Wabunge
Naye Mbunge wa Ukonga, Mheshimiwa Bakari Shingo ambaye amewawakilisha wabunge wa Dar es Salaam amesema,kliniki hii ni muhimu zaidi kwani itasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili katika nyanja mbalimbali.
Aidha, kwa niaba ya wabunge wenzake wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kikamilifu katika kuwahudumia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Shingo ametoa mfano kuwa, moja ya changamoto kubwa ya kisheria inayowakabili wananchi wa mkoa na jimbo lake kwa ujumla ni migogoro ya ardhi ambalo anaamini kuwa, kupitia wanasheria wabobezi wananchi watapata msaada wa kisheria bure.